VITUO VINAVYOPOKEA WAGENI VYATAKIWA KUJIANDAA KUKABILIANA NA MARADHI YA MRIPUKO

Mfanyakazi wa Kitengo cha Afya cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Amani Karume akimfanyia uchunguzi wa afya Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed alipotembelea kuangalia matayarisho ya kukabiliana na maradhi ya mripuko.

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed amewataka wafanyakazi wa Uwaja wa ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Amani Karume na Bandari kuu ya Malindi kuweka tahadhari kubwa na kujiandaa kukabilinana na  maradhi ya mripuko yatakapo tokea.

Amesema vituo hivyo viwili ni sehemu muhimu katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar hivyo zinatakiwa kuendelea kuwa salama ili wasafiri wawe na uhakika wa afya zao wanapoingia nchini.

Waziri wa Afya alitoa maelekezo hayo alipotembelea Kitengo cha Afya cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar na Bandari ya Malindi kuangalia maandalizi ya kukabiliana na maradhi ya kuambukiza ambayo baadhi ya nchi jirani maradhi kama Ebola yameanza kuripotiwa.

Amewahakikishia wananachi kuwa Tanzania hakujawa na tishio la maradhi hayo lakini tahadhari inatakiwa kuwepo kwa vile wasafiri kutoka nchi zilizopata maradhi hayo huingia nchini kwa shughuli mbali mbali.

Alisema kwa kipindi kirefu maradhi ya Ebola yalikuwa yakishambulia nchi za Afrika ya Magharibi lakini katika siku za karibuni yameanza kuonekana katika nchi jirani za Afrika Mashariki.

Amewataka wafanyakazi wa vitengo vyote vya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na Bandarini kufanyakazi kwa ushirikiano mkubwa hasa linapotokea tatizo linaloweza kusababisha madhara kwa wasafiri na wananchi.

”Nchi yetu inategemea Utalii kwa uchumi wake na Kiwanja cha ndege na Bandarini ni milango mikubwa ya kupokea na kusafirisha Watalii hivyo tunatakiwa kuwahakikishia afya zao wakati wote,” alisisitiza Waziri Hamad Rashid Mohamed.

Aliupongeza uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Shirika la Bandari Zanzibar kwa maandalizi aliyoyaona ya kukabiliana na tishio lolote la maradhi ya mlipuko na kuwashauri kuendelea kuwafanyia uchunguzi wageni wote wanaotoka katika nchi ambazo maradhi hayo yameanza kuonekana.

Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege Zanzibar Bi. Zaina Ibrahim Mwalukota amemuhakikishia Waziri wa Afya kwamba wamejipanga kuhakikisha wageni wote wanafanyiwa uchunguzi wa afya na watakaobanikia kuwa na matatizo kumewekwa taratibu mzuri wa kuhudumiwa.

Alisema Kitengo cha Afya cha Uwanja wa Ndege kinafanya kazi nzuri ya kuwafanyia uchunguzi wasafiri wanaoingia nchini lakini alimuomba Waziri kuwapatia gari la wagonjwa (Ambulance) ili liweze kutumika itakapotokea dharura.

Loading