JENGO KONGWE LA HOSPITALI YA MNAZIMMOJA KUFANYIWA MATENGENEZA YA PAA NA DARI

Jengo kongwe la Hospitali Kuu ya Mnazimmoja linatarajiwa kufanyiwa matengenezo ya paa na dari kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Jumatano ijayo kutokna na kuvuja kwa muda kirefu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake, Msemaji Mkuu wa Hospitali ya Mnazimmoja Hassan Makame alisema kuvuja kwa jengo hilo kumepelekea sehemu kubwa ya dari kuharibika na kuhitaji matengenezo makubwa.

Alisema kutokana na ushauri uliotolewa na Mamlaka ya Mji Mkongwe, paa la Hospitali hiyo halitavunjwa bali litafanyiwa marekebisho sehemu za misumari inayovujisha na kuwekwa misumari mipya.

Alisema hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na Wizara ya Afya kuhakikisha Hospitali hiyo inafikia lengo la kuwa Hospitali ya rufaa.

Hassan aliwata wananchi kutoa ushirikiano kwa uongozi wa Hospitali kutokana na usumbufu utakaojitokeza kwa sababu wagonjwa ambao hawatakuwa na sababu kubwa ya kulazwa wataruhusiwa na upasuaji unaoweza kusubiri utasogezwa siku za mbele.

Hata hivyo Msemaji huyo aliwahakikishia wananchi kuwa upasuaji wa dharura na ambao hauwezi kusubiri utafanywa wakati wote wa  matengenezo.

Katika kudumisha hali ya usafi ndani ya wodi za wagonjwa, msemaji Hassan aliwashauri jamaa wa wagonjwa wanaolazwa kuacha tabia ya kuchukua mizigo mingi kwani huduma nyingi zinapatikana hapo hapo.

Matengenezo ya paa na dari katika Hospitali kongwe ya Mnazimmoja  yatafanywa na Kampuni ya Ujenzi ya Mamba na yatagharimu shilingi milioni 154 hadi yatakapo kamilika.

Loading